SIASA NA MADARAKA
“ Mimi ni mwanazuoni, sio mwanasiasa, ingawa ninapenda siasa. Huwa wanasiasa hawapendi siasa, wanapenda madaraka.” Ni maneno ya Prof. Shivji ikiwa ni sehemu ya hotuba yake katika kongamano la kwanza la katiba lililo andaliwa na wanataaluma wa chuo kikuu cha Dar es salaam UDASA lililo fanyika katika ukumbi wa Nkuruma na kurushwa mojakwamoja na kituo cha ITV. Kongamano hilo lilihudhuriwa na waandishi wa habari wasomi, wanasiasa, wafanyabiashara, wakulima, na hata raiya wa nchi ya kenya na watu mbalimbali ambao ilikuwa ni vigumu kuwatambua. Mimi katika makala hii sito zungumzia mjadala juu ya katiba, ila nimevutiwa na maneno ya prof. ambayo yamenisukuma kufanya uchambuzi na kutaka kujua kuwa ni jinsigani mtu anaweza kuwa hapendi kitufulani lakini atajihusisha nacho ili apate kitu kingine kinacho tokana na kitu hicho asicho penda. Kwa mifano ya kawaida, mtu anaweza akawa mwizi, lakini hapendi kuwa mwizi ila anapenda kuwa na mali. Au mwanamke anaweza kuwa anapenda mtoto, lakini hapendi kuwa mja mzito. Pia mwanafunzi anaweza kuwa hapendi kujisomea lakini anapenda kufaulu. Ninaweza kutoa mifano mingi ambayo inaendana na kauli ya prof. Shivji lakini katika mifano hiyo hebu jaribu kuchambua jambo au kitu watu wengi ambacho hawakipendi huwa ni kigumu au kinaleta karaha na pia kinaweza kumuweka mtu katika hatari. Katika mifano yangu ukiangalia mambo kama wizi unaweza kumuweka mtu katika hatari ya kufa au kufungwa na ndo maana mtu anaweza akasema hapendi wizi lakini yeye ni mwizi kwasababu anataka mali, ujauzito pia ni njia ambayo mwanamke anaupitia ili apate mtoto, lakini ni hatari kwani ujauzito wakati mwingine unaweza ukampelekea mwanamke katika hatari ya kupoteza maisha au kupata matatizo mengine yatokanayo na huo ujauzito, pia baadhi ya wanawake hushindwa kufanya shughuli zao muhimu wakiwa katika hali hii ya uja ujzito. Swala la kujisomea kwakweli ni muhimu kwa mwanafunzi lakini huwa linakera kidogo haswa kwa somo ambalo hulipendi lakini ni lazima kulisoma somo hilo. Kila mwanafunzi ambaye anajua wajibu na umuhimu wake wa kuwa shuleni anapenda kufaulu, lakini wanafunzi wengi hawapendi kusoma kwasabasbu tu masomo hayavutii.
MAHUSIANO YA WAONGOZI NA WAONGOZWA KATIKA SIASA
Kama ilivyoelezwa kabla, msingi mzima wa siasa katika maongozi ya tawala za kidemokrasia (na hata baadhi ya tawala za kidikteta hudai hivyo hivyo) unahusu ridhaa (mandate) ambayo wanaoongozwa huitoa kwa waongozi na hivyo kuwapa uhalali wa kusimamia mambo yao. Lakini ridhaa hiyo haitolewi hivi hivi tu, inaambatana na amana (trust) kwamba waongozi watatekeleza dhamana (obligations) na wajibu (duties) wao kwa makubaliano na maelewano ya kufuata barabara na kuheshimu ipasavyo kanuni na maadili (norms, values and tastes) fulani yanayoitambulisha na kuiongoza jamii husika. Marcus Tullius Cicero katika kitabu chake cha The Republic, kama kilivyonukuliwa na Chris Paten kwenye kitabu chake, East and West, Uk. 146 anayaeleza mahusiano haya kama ifuatavyo: “Well, then, a commonwealth is the property of a people. But a people is not any collection of human beings brought together in any sort of way, but an assemblage of people in large numbers associated in an agreement with respect to justice and a partnership for the common good. The first cause of such an association is not so much the weakness of the individual as a certain social spirit which nature has implanted in man.” Katika mifumo ya kileo, mambo haya huwekwa katika katiba na sheria za nchi ambazo zinajumuisha misingi ya jumla ya maongozi ya nchi, na pia huwekwa katika ilani (manifesto) za uchaguzi ambazo vyama vya siasa huziwasilisha kwa wapiga kura ili kupata ridhaa yao katika kuamua sera zitakazofuatwa na Serikali katika kipindi maalum kilichowekwa (hapa kwetu ni miaka mitano) baada ya uchaguzi kukamilika. Vitu hivyo viwili – Katiba na Ilani – huwa ndiyo mkataba baina ya waongozi na waongozwa katika uendeshaji wa nchi na Serikali. Dhana ya demokrasia ambayo ilianzishwa na Wagiriki na sasa inabeba misingi ya kileo ya maongozi ya nchi inasisitiza suala hilo la mapatano yanayoongoza nchi baina ya waongozi na waongozwa. John Uhr katika kijitabu chake, Creating a Culture of Integrity, ameifafanua vyema tafsiri hii ya demokrasia pale aliposema: “Democracy at its simplest refers to government by the people, carried out in the interests of the whole community. Democracy is often called ‘people power’. The central democratic idea is popular sovereignty: the idea that the people are the ultimate sovereign and that ‘good government’ demands that those who govern do so as representatives of the people whose welfare they hold in trust. Popular sovereignty is translated into practice by the people’s right to vote, and to stand for office, and so determine who governs. The legitimacy of democratic governments flows from their dependence on the freely-expressed consent of their citizens. Elections provide one important opportunity for the expression of popular consent. Elections also serve an important accountability function by reminding those who govern that they are meant to put the public good ahead of their own particular interests. Elections are thus important tests of accountability for governments as well as tests of popular consent to either the serving government or to alternative parties or individuals seeking a representative role.” Ndiyo maana wanafalsafa huiita Katiba kuwa ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa. Kwa maneno mengine, ni mkataba wa amana (trust) ambao unaongoza mahusiano kati ya waongozi na waongozwa. Wakati mwengine mahusiano haya pia huja katika mfumo wa Mkataba wa Kijamii (Social Contract) kama ilivyokuwa Ufaransa baada ya Mapinduzi ambao uliweka misingi ya Uhuru, Usawa na Udugu (Liberty, Equality and Fraternity). Katika katiba, msingi wa mahusiano hayo ya waongozi na waongozwa huwekwa katika Utangulizi (Preamble). Kwa mfano, Utangulizi wa Katiba ya Zanzibar unaeleza nia ya wenye katiba (sponsors of this constitution) ambao ni wananchi juu ya vipi Zanzibar iongozwe. Hivyo madaraka liliyo nayo Baraza la Wawakilishi, ambalo ndilo lililotunga katiba hiyo mwaka 1984, yanatokana na wananchi na kwamba Baraza linayashikilia madaraka hayo kama amana (trust) kwa niaba ya wananchi hao. Sehemu ya utangulizi huo inabainisha: “NA KWA KUWA SISI, Wananchi wa Zanzibar tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani; NA KWA KUWA misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo Serikali yake husimamiwa na Baraza la Wawakilishi lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowakilisha wananchi, na pia yenye Mahkama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa ukamilifu;
UADILIFU WA UONGOZI KATIKA SIASA NI UPI?
Mtu angeweza kusema kuwa maelezo yaliyotangulia hayatoi nafasi ya kuwepo uadilifu wa uongozi katika siasa kwa sababu ya maumbile yake. Mtu anapotazama maisha ya kila siku ya wanasiasa ataiona siasa imejikita katika kukimbilia na kupigania ulwa, fursa na ushawishi kwa malengo ya kujilimbikizia uwezo wa maamuzi na wa utajiri binafsi usiohojiwa kuliko kuzingatia kwamba siasa ni utumishi wa dhati na uliotukuka kwa umma uliozindukana. Huo ni udhaifu wa mwanadamu ambao hapaswi kuupa nafasi iwapo anazingatia uadilifu wa uongozi. Mwanafalsafa maarufu wa Kichina, Confucius, anatwambia katika The Analects of Confucius, 4.5: ‘The Master said: ‘Riches and rank are what every man craves; yet if the only way to obtain them goes against his principles, he should desist from such a pursuit.’ ‘Utajiri na vyeo ndivyo vitu ambavyo kila bianadamu anavitamani; lakini ikiwa njia ya kuvipata ni kwa kwenda kinyume na misingi yake, anapaswa ajiepushe navyo.’ Hata hivyo, si sahihi wala si haki kudhani kwamba siasa hutumiwa kwa malengo ya kutimiza haja binafsi kama hizo tu. Siasa bado imebaki kuwa fani muhimu ya kuwatumikia wananchi na ina misingi na maadili yake kama zilivyo fani nyengine. Iwapo wachezaji (iwe wengi au wachache) hawaheshimu misingi na maadili hayo, tatizo litakuwa ni la wanasiasa na siyo la siasa. Mmojawapo wa wasomi wanaoheshimika hapa Tanzania, Profesa Issa Shivji, aliwahi kuiambia Tume ya Nyalali mwaka 1991 kuwa, “Wanafalsafa wanapenda siasa lakini hawapendi madaraka, wanasiasa hawapendi siasa, wanapenda madaraka.” Lakini basi ni yepi hayo maadili ya uongozi wa kisiasa? Si rahisi kuchukua nadharia moja ukaitumia kuweka maadili ya uongozi wa kisiasa lakini waraka huu ukisaidiwa na maandiko mbali mbali ya wanafalsafa na wachambuzi wa masuala ya siasa unapendekeza kutafakari kwa pamoja vigezo vifuatavyo vya kiongozi muadilifu katika siasa. • Kiongozi anaongoza, haongozwi Kwa mtazamo wangu, msingi wa kwanza wa uadilifu wa uongozi katika siasa unapaswa uwe ule uliomo katika neno lenyewe “kiongozi” kwa maana ya kuonesha njia. Msingi huu unaaminisha kuwa kiongozi kwanza awe muadilifu kwa uongozi wake na hivyo awe anaongoza badala ya kuongozwa. Kiongozi katika jamii anatakiwa awe ametambuliwa na kukubalika na wanajamii kutokana na sifa fulani alizo nazo zinazomtofautisha na wengine na hivyo kuaminika kuwa anaweza kuonesha njia kwa wale wanaomuona ana uwezo huo. Uongozi kama huu mara nyingi huambatana na mvuto wa maumbile (charisma) inayowapelekea wanajamii kwa hiyari zao wenyewe kujikubalisha na kutoa utiifu wao kwa yule wanayemuona kiongozi wao. Kiongozi wa aina hii huwa na kipawa na kipaji fulani kinachompa nafasi ya kuona zaidi kuliko wengine lakini pia akitumia habari na taarifa ambazo wengine hawazipati kuweza kufikia maamuzi yenye maslahi na jamii nzima. Rudolph Giuliani, aliyekuwa Meya wa New York wakati wa matukio ya Septemba 11, akiandika kuhusu Uongozi kwenye kitabu chake, ‘Leadership’, Uk. 207 anasema: “A leader is chosen because whoever put him there trusts his judgment, character, and intelligence – not his poll-taking skills. It’s a leader’s duty to act on those attributes.” ‘Kiongozi huchaguliwa kwa kuwa yeyote anayemuweka pale huwa anaamini maamuzi, tabia na uwezo wa maarifa yake – siyo ujuzi wa kufuata maoni. Ni wajibu wa kiongozi kuchukua hatua kufuatana na sifa hizo.’ Kwa nafasi hiyo, kiongozi muadilifu hakubali kufuata upepo wa maoni ya jamii tu (opinion polls) ambayo huyumba kulingana na wakati na mara nyingi hayazingatii maslahi ya muda mrefu. Kiongozi anayesikiliza mdundo na kisha kufanya maamuzi yake kulingana na ‘mdundo’ uendavyo (populist) huwa amekimbia dhamana kuu ya uongozi na huishia kuyumba na kuiyumbisha jamii anayoiongoza. Kusema hivi hakuna maana ya kiongozi kuwa dikteta na kutosikiliza maoni ya anaowaongoza. La hasha! Maoni na ushauri ni muhimu, lakini hayo hayondoshi dhamana ya kiongozi kutumia kipaji, kipawa, taarifa na busara za uongozi kufanya maamuzi na kuyasimamia. Confucius anatwambia katika The Analects of Confucius, 2.24: ‘The Master said: ‘To worship gods that are not yours, that is toadyism. Not to act when justice commands, that is cowardice.’ ‘Kuabudu miungu isiyo yako, huko ni kujikomba. Kutochukua hatua pale uadilifu unapokutaka ufanye hivyo, huo ni woga.’ • Kiongozi anapaswa azingatie maslahi ya nchi na watu wake hata kama watu wataona anayoyafanya hayana maslahi nao kutokana na ufinyu wa taarifa Uwezo na madaraka huambatana na dhamana (power comes with responsibility). Hivyo, dhana ya kiongozi kuongoza badala ya kuongozwa inaambatana pia na dhamana ya kuhakikisha na kujiridhisha kuwa mara zote maamuzi anayoyatoa na kuyasimamia yamefanywa kwa maslahi ya nchi na watu wake. Mara nyengine hali hii huambatana na wale anaowaongoza kuona kuwa maamuzi hayo si sahihi na hayana maslahi nao lakini hayo huweza kusababishwa na waongozwa kutokuwa na taarifa ambazo kiongozi kwa nafasi yake huwa nazo. Hivyo, unabaki kuwa wajibu muhimu wa uadilifu wa uongozi katika siasa kuwa kila maamuzi yanayofanywa yawe yametokana na kujiridhisha kwa kiongozi huyo kuwa yanawakilisha maslahi bora zaidi kwa anaowaongoza. Yanaweza kuwa na athari za muda mfupi na mara nyengine kuwa na machungu lakini alimradi tu machungu hayo ni ya muda mfupi, uadilifu wa uongozi unadai kiongozi kutoyumba wala kutetereka katika kuyatetea. • Kiongozi anatakiwa awe mfano kwa anaowaongoza Kuweza kuyafanikisha mambo hayo mawili yaliyotajwa hapo juu, kiongozi anapaswa kuwa mfano bora kwa anaowaongoza kwa kuwa na ‘moral command’ ambayo huja kwa yeye mwenyewe kuyafuata na kuonekana anayafuata yale anayoyadai kutoka kwa anaowaongoza. Kwa maneno mengine, kiongozi anatakiwa atembee juu ya maneno yake (A leader has to walk his talk). Kwa mfano, huwezi ukawataka raia wafuate sheria wakati wewe mwenyewe unaongoza kwa kuvunja sheria, huwezi kuwataka raia wasijiingizie katika rushwa wakati wewe unakula na kunywa, unalala na kuamka na rushwa. Huwezi kuwaambia raia wapambane wakati wewe unakimbia vita. Confucius anasema katika The Analects of Confucius, 14.27 kwamba ‘A gentleman would be ashamed should his deeds not match his words’ yaani muungwana anapaswa kuona aibu iwapo vitendo vyake havilingani na kauli zake. • Kiongozi anapaswa azingatie haki na uadilifu kwa anaowaongoza (wanaomkubali na wasiomkubali) Msingi wa uongozi ni uadilifu. Kiongozi anapaswa kusimamia haki na uadilifu kwa wote anaowaongoza bila ya upendeleo wala chuki. Haki na uadilifu huu uonekane katika usawa mbele ya sheria, kufaidi fursa za nchi kwa usawa, na kuwepo kwa urari wa maendeleo kati ya sehemu zote za nchi. Isitokee sehemu ya jamii au nchi ikahisi inatengwa, kudharauliwa, kubaguliwa, kunyanyaswa au kukandamizwa. Watu wote wajione wana haki na fursa sawa. Waongozwa wakiona hayo na kuridhika, utiifu wao kwa waongozi huwa hauna shaka, na hutokana na hiyari ya kweli. Na kama wasemavyo wahenga, hiyari yashinda utumwa. • Kiongozi azingatie umoja wa anaowaongoza Kiongozi muadilifu mara zote atahakikisha kunakuwepo umoja miongoni mwa anaowaongoza kwani huwa anauhitaji umoja huo kushajiisha na kuchechemua maendeleo ya nchi na watu wake. Kiongozi muadilifu hawagawi anaowaongoza kwa kuwa hana sababu ya kufanya hivyo. Kwa hakika umoja wa Taifa analoliongoza ni fakhari ya kiongozi muadilifu. Kiongozi anayewagawa watu ni muovu, huwa hawaamini anaowaongoza na huwaogopa. Ili kujihami yeye na madaraka aliyo nayo, kiongozi muovu huishia kuwagawa watu wake kwa kupandikiza chuki na fitina. Isitoshe, mara nyingi misingi ya umoja katika nchi humong’onyoka ikiwa ni matokeo ya kiongozi kushindwa kusimamia haki na uadilifu. • Kiongozi azingatie amani na utulivu katika nchi Kama ilivyo kwa umoja wa kitaifa, kiongozi muadilifu pia hufanya kila bidii kuhakikisha amani na utulivu wa kweli katika nchi vinapatikana. Amani na utulivu ni chachu ya wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao kujiletea maendeleo. Maendeleo hayaji mahala penye magomvi na hasama. Lakini na amani na utulivu pia haviji mahala pasipo na haki na uadilifu. Uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi hupelekea hasara ya maisha na mali ya watu na hayo hayawi malengo ya uongozi muadilifu katika nchi. • Kiongozi asikubali kuona ukandamizaji wa aina yoyote Yaliyotajwa hapo juu – haki, uadilifu, umoja, amani na utulivu – yanapatikana pale ambapo hakuna ukandamizaji wa aina yoyote dhidi ya raia. Uadilifu wa uongozi katika siasa unadai kiongozi kuchukua hatua za makusudi, za dharura na za haraka kuondosha ukandamizaji wa aina yoyote ile iwapo utathibitika au hata kudhaniwa tu. Wanasayansi wa siasa wanasema siasa ni mchezo wa dhana au hisia (politics is a game of perception). Kwa hivyo haki inapaswa sio tu itendeke bali ionekane kuwa inatendeka ili kuodosha uwezekano, hata kama ni mdogo kiasi gani, wa kuhisiwa kuwepo na ukandamizaji dhidi ya wengine. Kwa kuazima tena falsafa za Confucius kutoka kwenye The Analects of Confucius, 15.24, anasema: ‘Zigong asked: ‘Is there any single word that could guide one’s entire life?’ The Master said: ‘Should it not be reciprocity? What you do not wish for yourself, do not do to others.’ ‘Zigong aliuliza: ‘Je, kuna neno moja tu linaloweza kumuongoza mtu maisha yake yote?’ Mwalimu akasema: ‘Lisiwe ni marejesho? Yaani kile usichokipendelea nafsi yako, usiwafanyie wengine.’ • Kiongozi awe muumini wa kweli wa demokrasia Jamii siku zote haiachi kuwa na mgongano wa fikra, na mgongano huu ni muhimu na unahitajika katika kuipeleka jamii hiyo mbele. Fikra zinapogongana na kushindanishwa hupelekea hoja madhubuti kuibuka na hivyo maamuzi kufikiwa kwa kuzingatia nguvu ya hoja na fikra bora. Uadilifu wa uongozi unadai kuheshimu nguvu ya hoja na fikra bora na hayo yanaweza kupatikana tu iwapo nchi inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia. Hivyo, katika kutoa uongozi sahihi, kwa kuzingatia maslahi bora ya nchi na watu wake, haki, uadilifu, umoja, amani na utulivu, hapana budi kwa kiongozi kuiamini, kuiheshimu na kuifuata barabara misingi ya kidemokrasia. Kwa maneno ya Confucius tena kutoka The Analects of Confucius, 13.15: ‘Is there one single maxim that could ruin a country?’ Confucius replied: ‘Mere words could not achieve this. There is this saying, however: “The only pleasure of being a prince is never having to suffer contradiction.” If you are right and no one contradicts you, that’s fine; but if you are wrong and no one contradicts you – is this not almost a case of “one single maxim that could ruin a country”?’ ‘Je, kuna methali moja tu inayoweza kuifisidi nchi?’ Confucius alijibu: ‘Maneno matupu hayawezi kulifanikisha hilo. Uko usemi huu, hata hivyo: “Furaha pekee ya kuwa mwana mfalme ni kutopingwa.” Ikiwa utakuwa sahihi na hakuna anayekupinga, hiyo ni sawa; lakini ukiwa makosani na hakuna anayekupinga – je, hii haiwi aina ya “methali moja tu inayoweza kuifisidi nchi”?’ • Kiongozi anapaswa kuwajibika kwa yanayotendwa kwa jina lake Pamoja na kuzingatia yote yaliyotajwa hapo juu, bado binadamu si mkamilifu na kwa vyovyote vile hufikia mahala akafanya maamuzi ambayo si sahihi hata kama yalifanywa kwa nia njema na kwa kuzingatia taarifa zilizopatikana wakati maamuzi hayo yanafanywa. Hayo yanaeleweka na kiongozi muadilifu anapaswa kuyakubali. Hata hivyo, inapotokezea maamuzi yanayofanywa na dola au taasisi yoyote yakaleta madhara au yakasababisha kuchafua jina jema la wadhifa ambao kiongozi wa kisiasa anaushikilia, basi uadilifu wa uongozi unamtaka yule aliyesababisha hayo au ambaye maamuzi yanayohusika yalifanywa kwa jina lake awajibike. Kwa mtazamo wangu, hiki ndiyo kilele na kigezo kikuu cha uadilifu wa uongozi katika siasa. Kukubali kubeba dhamana kwa madhara yaliyotokana na maamuzi yako au yaliyofanywa kwa jina lako. • Kiongozi awapende anaowaongoza Itadhihirika mpaka sasa kwamba dhima anazotwishwa nazo kiongozi wa siasa ni kubwa na zinahitaji uimara wa nafsi katika kuzisimamia. Yote yanayofanywa hufanywa kwa jina la watu (in the name of the people). Imeonekana kwa mfano, mara nyengine kiongozi hulazimika kufanya maamuzi yasiyopendeza kwa watu wake kwa wakati fulani lakini akayashikilia kwa kujiridhisha kuwa yana maslahi na anaowaongoza. Uamuzi kama huo huwa si mwepesi. Hapo basi, kipimo kikubwa ni mapenzi ya kiongozi kwa anaowaongoza. Uadilifu unataka kiongozi awe na mapenzi, imani na huruma kwa anaowaongoza. Uadilifu pia unamtaka kiongozi awape nafasi wananchi wake wafanye yale wayapendayo alimradi yana maslahi nao na hayaathiri maslahi ya jamii. Confucius anatufundisha tena kwenye The Analects of Confucius, 20.2: ‘Zizhang said: ‘How can one be generous without having to spend?’ The Master said: ‘If you let the people pursue what is beneficial for them, aren’t you being generous without having to spend?’ ‘Zizhang alisema: ‘Vipi mtu anaweza kuwa karimu pasina kulazimika kutumia?’ Mwalimu akajibu: ‘Ukiwaachia (kuwapa uhuru) watu wafanye yale yanayowafaidisha, huwi karimu pasina kulazimika kutumia?’ Raia wakiridhika na hilo wanaweza kumwelewa kiongozi wao hata anapofanya maamuzi yanayoonekana kuwa magumu na machungu kwa wakati fulani. Nyoyo za raia zinapokuwa tulivu na roho zao zikawakinai wanaowaongoza, hapahitajiki nguvu za dola kuhakikisha utiifu wao. Kiwango hicho kikifikiwa, kiongozi huwa hatawali viwiliwili bali anatawala nyoyo za anaowaongoza. • Kiongozi aheshimu misingi ya uongozi wa pamoja Uongozi ni dhamana. Maamuzi makubwa yanapofanywa kwa jina la watu yanatakiwa yazingatie maslahi yao. Serikali au chama cha siasa huchangiwa nguvu zake kwa ridhaa inayotolewa na raia au wanachama. Wao huchagua viongozi wakuu na pia huchagua wawakilishi wao katika vyombo vinavyofanya maamuzi yanayowahusu. Baadhi ya wawakilishi hao hupewa dhamana ya kusaidiana na kiongozi mkuu katika uongozi na uendeshaji wa Serikali au chama cha siasa. Katika utaratibu huo, maamuzi hufanywa kwa pamoja. Kiongozi muadilifu siyo tu anapaswa kulifahamu hilo bali pia anatakiwa aheshimu misingi ya uongozi wa pamoja. Anaweza kutofautiana na wenzake katika kufikia maamuzi, lakini alimradi mwisho wa hoja zote maamuzi yamefanywa kwa taratibu za kidemokrasia, anapaswa aheshimu maamuzi hayo na akubali misingi ya uongozi na uwajibikaji wa pamoja. • Kiongozi awe na busara na hekima Maamuzi ya mtu binafsi mara nyingi humuathiri yeye binafsi au labda na watu wachache waliomzunguka. Maamuzi ya kiongozi wa kisiasa huathiri taifa zima. Changamoto za uongozi kama nilivyojaribu kuzifafanua hapa zinahitaji utulivu katika kufikia maamuzi na kuyasimamia. Jazba na hamasa mara nyingi hupelekea maamuzi ya pupa, yasiyozingatia hali halisi ya mambo na mara nyingi yenye manufaa (kama yatapatikana) ya muda mfupi tu. Kinyume chake, busara na hekima huzaa maamuzi yanayotokana na tafakuri ya kina, yanayozingatia hali halisi ya mambo na maslahi na manufaa ya muda mrefu. Kiongozi muadilifu anatakiwa ayaone haya na ayazigatie kwa kila hatua anayochukua. • Kiongozi awe anaijua jamii yake vilivyo Orodha ya sifa na vigezo vya uadilifu wa uongozi imekuwa refu. Na wala sikusudii kusema mimi ni mjuzi (authority) wa fani ya uongozi wa kisiasa. Lakini uzoefu umenifundisha kuwa hata ukiyazingatia yote hayo, kama kiongozi huijui vyema jamii unayoiongoza, unaweza ukajikuta unafanya maamuzi au kuchukua hatua ambazo hazizingatii uhalisi wa mambo na hivyo kutofikia malengo yaliyokusudiwa, kama si kuirudisha nyuma dhamira nzima ya taasisi unayoiongoza. Wafuasi mara nyingi hutawaliwa na jazba na hamasa zinazotokana na uoni wao wa mambo kulingana na kiasi cha uelewa wao. Wafuasi hao wanawakilisha makundi yenye maslahi tofauti katika jamii. Kila kundi hudhani na hujionesha kuwa fikra zake ndizo zinazowakilisha jamii nzima kwa ujumla. Mara nyingi huzipandisha mno (overestimate) nguvu zao kuliko ukweli ulivyo na mara chache huzidharau na kuzidunisha (underestimate) nguvu hizo. Kiongozi mzuri ni yule anayeielewa vyema jamii yake na ambaye ameisoma na kuijua vilivyo nguvu halisi ya jamii hiyo. Kiongozi kama huyo hachukuliwi na jazba za wafuasi kiasi cha kutoona udhaifu wao lakini pia hapuuzi dhamira zao kiasi cha kutoona nguvu waliyo nayo. Akifika hapo, hatokwenda mbele wakati wafuasi hawako naye wala hatobaki nyuma wakati wafuasi wameshatangulia mbele. Kiongozi anapaswa kuwa kiongozi anayekwenda sambamba na wafuasi wake kwa kujua nguvu na udhaifu wao. Uadilifu wa uongozi hauwezi kufikiwa bila ya kulitambua hilo. Confucius kwenye The Analects of Confucius, 10.12 anasema, ‘Do not sit on a mat that is not straight,’ yaani usikae juu ya mkeka ambao haujakunjuliwa. Kutokana na hisia mbaya zilizojengeka, imekuwa ni kawaida kuwasikia watu wakisema hakuna kitu kinachoitwa ‘uadilifu katika siasa’. Wengine husema hiyo ni hadithi ya ‘Kusaidikika’ au ndoto za Alinacha. Mimi nina mawazo tofauti. Naamini kuwa uadilifu ndiyo unapaswa kuwa msingi wa siasa, msingi wa maongozi ya kisiasa. Ikiwa siasa haiwezi kuwa na uadilifu basi itakuwa imepoteza uhalali wake wa kuwa ni njia ya kuwatumikia watu. Utumishi wa umma ni utumishi uliotukuka na unapaswa ubakie hivyo. Na msingi wake ni uadilifu. Wanasheria wana msemo wa kusisitiza umuhimu au tuseme ulazima wa kufanya uadilifu usemao, “Let justice be done even if heaven falls” yaani “Haki na itendeke hata kama mbingu zitaanguka”. Ninavyoamini mimi ni kuwa msisitizo wa usemi huu uko katika kinyume chake yaani haki inapotendeka basi hata mbingu huzidi uimara wake. Kwa wanaoamini katika dini wanajua kuwa Uadilifu ndiyo msingi wa Ufalme wa Mbinguni. Lakini wakati kwa Mahakimu na wanasheria, msingi wa uadilifu ni katika kufuata sheria kama zilivyo, kwa maneno mengine uhalali (legality), kwa wanasiasa msingi mkuu wa uadilifu unapaswa kuwa ni kutenda haki (legitimacy) katika maamuzi hayo. Na kazi ya kuhakikisha hayo si nyepesi lakini si kitu kisichomkinika. Kama alivyosema Jaji mmoja wa Mahkama Kuu ya Uingereza akitoa maoni yake kuhusiana na hukumu ya Mahkama ya Kimataifa ya The Hague kuhusiana na shauri la ubaguzi wa rangi Afrika Kusini ambalo lilihusu zaidi mfumo wa siasa kuliko utekelezaji wa sheria pale aliposema, “It is a typical case of legality against legitimacy” yaani “Ni kesi dhahiri ya sheria dhidi ya haki”. Kwa hivyo, kiongozi wa siasa ana dhima na dhamana ya kuhakikisha uadilifu na siyo kujificha nyuma ya pazia la sheria (kandamizi). Anaweza kufikia hapo kwa kuzingatia vigezo tulivyojaribu kuviorodhesha katika waraka huu.
MATOKEO YA KUPUUZWA MISINGI YA UONGOZI WA UADILIFU KATIKA SIASA
Dunia kwa ujumla hivi sasa inashuhudia mmong’onyoko wa imani kwa wanasiasa. Wananchi wanahisi wamedanganywa sana na kusalitiwa kiasi cha kuona kuwa wanasiasa wote ni sawa sawa, jora moja mkasi mmoja. Hawaamini kama kutakuwa na tofauti hata kama watabadilisha uongozi kwani kila waliyemuanini amewaangusha. Imani kwa viongozi ikiondoka basi na ule msingi wa amana (trust) ambao, kama tulivyoona, ndiyo msingi mkuu wa maongozi ya nchi nao hundoka. Hali hiyo ya kupoteza matumaini ni hatari kwa sababu bado hakuna mbadala wa siasa kama njia ya kuufikia uongozi wa nchi. Mfano mzuri sana wa karibuni wa jinsi maamuzi yasiyozingatia misingi ya uadilifu yanavyoathiri mitazamo ya raia kwa viongozi wao unapatikana kwa Waziri Mkuu wa zamani Uingereza, Tony Blair. Likifanya tathmini ya mtazamo wa raia kwa kiongozi huyo ambaye nilibahatika nikiwa Uingereza mwaka 1997 kushuhudia jinsi alivyopendwa na kuaminiwa na Waingereza, jarida linaloheshimika la The Economist la Mei 12 – 18 2007, linaandika: “Few Britons, it seems will shed a tear when Tony Blair leaves the stage on June 27th after a decade as prime minister, as he finally said this week he would. Opinion polls have long suggested that he is unpopular. On May 3rd local and regional elections gave voters a last chance to give Mr Blair a good kicking. They took it with both feet, handing power to Conservatives, Scottish Nationalists, Welsh nationalists, anybody but distrusted Labour. Most wish he had gone last year – an opinion shared by his likely heir, Gordon Brown, who now faces a mighty struggle against David Cameron’s Tories. Either Britons are an ungrateful lot, or Mr Blair deserves his shabby send-off for having delivered too little and disappointed too much. The truth, as usual, is more complicated. … [Mr Blair], after all, was the most gifted politician of his generation – certainly in Europe and (depending on your opinion of the foxier but less disciplined Bill Clinton) perhaps wider than that. Before coming to power Mr Blair already had one enormous achievement to his name: dragging the Labour Party to the electable centre. In 1997 he had not just a big parliamentary majority but a country that wanted what he wanted – an economy that combined the hard-won gains of Thatcherism with a greater emphasis on social justice and modernised public services. How could he fail?” Tony Blair ‘alilewa’ na imani aliyopewa na Waingereza, akajiamini kupita kiasi kwamba angeweza kufanya lolote na bado akaendelea kupendwa, akadhani anaweza kwenda mbele na kuuwacha umma nyuma, akashindwa kufanya mahesabu ya maslahi bora kwa Uingereza kwa wakati fulani, akaitia nchi vitani kwa taarifa zisizo sahihi na zilizopotoshwa kwa makusudi. Matokeo yake ni machungu siyo kwa Uingereza tu bali kwa ulimwengu mzima. Hiyo ndiyo athari ya kutozingatia uadilifu katika uongozi wa kisiasa. Hapa kwetu Zanzibar, mfano mzuri wa mwanasiasa aliyepoteza fursa adhimu kama hii nadhani ni Dk. Salmin Amour. Aliingia madarakani wakati Zanzibar imo katika mgawanyiko mkubwa wa kisiasa kufuatia Maalim Seif Sharif Hamad kuondolewa katika nafasi ya Waziri Kiongozi na baadaye kufukuzwa kutoka CCM na kuwekwa ndani kwa mashtaka ya kubambikiziwa. Watu wakampa nafasi ya kurejesha umoja na matumaini katika nchi. Alianza vizuri katika uwanja wa uchumi na kipindi chake kikashuhudia Maalim Seif kupewa dhamana na kutolewa kutoka gerezani, akaanzisha mawasiliano ya kimya kimya na Maalim Seif ambayo yalikusudiwa yalete siasa za maelewano. Ghafla akageuka. Mawasiliano yakakatika, akaanza mashambulizi makali na vitisho dhidi ya mwenzake na baadaye dhidi ya wapinzani wote, Zanzibar ikashuhudia utawala wa mkono wa chuma, na baada ya uchaguzi mkuu wa 1995, mgogoro mkubwa wa kisiasa. Hatimaye juhudi za Chief Emeka Anyaoku wa Jumuiya ya Madola zikaleta Muafaka mwaka 1999. Dk. Salmin akapata fursa ya pekee mwaka mmoja tu kabla ya kumaliza muda wake wa Urais kuwapa Wazanzibari zawadi ya umoja, amani na utulivu. Akatoa hotuba safi katika viwanja vya Ikulu, Juni 9, 1999 ambayo ikiambatana na kitendo chake cha kukumbatiana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, iliibadilisha Zanzibar na kubadilisha mahusiano ya wafuasi wa CCM na CUF ndani ya usiku mmoja tu. Akasema: “Lakini lazima tuseme wazi kabisa, tuelewane ili Muafaka huu uote mizizi na usonge mbele. Siwezi kuwa shahidi wa Muafaka ambao umehusisha watu wakubwa kama huyu mwenzetu Ndugu Anyaoku, kwa miaka minne, halafu baada ya siku tatu ukaelea na maji. Itakuwa haina maana yoyote. Dhamana itakuwa mimi na Maalim Seif, ama yeye au mimi. … Na mimi natamka nitautekeleza na kuusimamia Muafaka huu na maelewano haya kwa uwezo wangu wote, kwa sababu hapa hapana suala la ushindi kwamba fulani kashinda, fulani kashindwa. Hapa tunazungumzia nchi kwa hivyo sote tumeshinda.” Hakuishia hapo bali aliendelea kusisitiza: “Natumai kwamba kuanzia sasa, watu wa Tumbatu, watu wa Shangani, watu wa Malindi, watu wa Makunduchi, wa Kisiwa Panza, wa Mkoani, wa Mtambwe, wa Kidombo, wa kila mahali mtakuwa kitu kimoja kufanya kazi ya uzalendo wa taifa letu, maana uzalendo ni nchi. Chama ni ushabiki. Chama hupita, nchi haiondoki, kwa hivyo ukiamua kwamba usahau nchi ushikilie chama tu, ukagombana na watu, ukaleta uhasama, ukaleta chuki, chama kuna siku kitakuwa hakipo, nchi haiondoki, kwa hivyo lazima tutafautishe baina ya uzalendo na ushabiki. Kwa hivyo wakereketwa wale ambao jazba zimewakaa kila wakati watambue wakati wa ushabiki wa siasa sawa, ukifika uzalendo sote tuwe kitu kimoja, alie Dar es Salaam, tuwe kitu kimoja, alie Tanga kitu kimoja, alie Mombasa kitu kimoja, alie Dubai kitu kimoja, alie Denmark, alie Sweden, alie London sote kitu kimoja. Huu ndio uzalendo.” Matumaini haya yalipotezwa na nchi ikarudi katika mgogoro mkubwa zaidi pale Dk. Salmin Amour alipoyageuka maneno yake mwenyewe katika mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Kibanda Maiti, Zanzibar wiki moja tu baadaye. Majeraha ya kisiasa tuliyokuwa nayo kabla ya kufikiwa kwa Maridhiano ya Wazanzibari Novemba 5, mwaka jana yalitokana na kitendo hicho cha Dk. Salmin kuigeuka dhamira yake. Confucius anasema ‘A gentleman would be ashamed should his deeds not match his words’ yaani muungwana anapaswa kuona aibu iwapo vitendo vyake havilingani na kauli zake.
HITIMISHO
Uongozi wa kisiasa si jukumu dogo ingawa siku hizi unaonekana ndiyo kimbilio la kila aliyefeli maisha katika nchi yetu. Si ajabu basi ikawa dhima na dhamana za uongozi wa kisiasa zimekuwa haziheshimiwi na uadilifu umepotea. Lakini kama tulivyotangulia kusema, uongozi wa nchi unatokana na amana ambayo hutolewa na wananchi. Hivyo, badala ya wananchi kukata tamaa na viongozi wao, wanapaswa kubeba jukumu lao la kudai uadilifu huo ikiwa ni marejesho ya amana waliyotoa. Hiyo ni changamoto kwa wananchi. Kwa upande mwengine, viongozi wa kisiasa nao wanapaswa wachukue hatua kujisafisha na kusafisha nyumba zao ili kurejesha imani ya wananchi kwao na kwa uongozi wao. Msingi wa kufanya hivyo ni kujichunguza na kujisahihisha. Huo ndiyo unapaswa kuwa msingi hasa wa utawala wa kidemokrasia tunaoupigia chapuo kwamba tunaufuata. Fareed Zakaria, mchambuzi wa masuala ya siasa anayeheshimika ulimwenguni, katika kitabu chake ‘The Future of Freedom: Illiberal Democracy at Home and Abroad’, Uk.256 anasema: “Modern democracies will face difficult new challenges … and they will have to make their system work much better than it currently does. That means making democratic decision-making effective, reintegrating constitutional liberalism into the practice of democracy, rebuilding broken political institutions and civic associations. Perhaps most difficult of all, it requires that those with immense power in our societies embrace their responsibilities, lead, and set standards that are not only legal, but moral. Without this inner stuffing, democracy will become an empty shell, not simply inadequate but potentially dangerous, bringing with it the erosion of liberty, the manipulation of freedom, and the decay of a common life.” Turudi katika mstari kwa kuzingatia ipasavyo misingi ya uadilifu wa uongozi. Kuyafanikisha hayo, panahitajika mafahamiano mapya ya mahusiano kati ya waongozi na wangozwa. Haya yanaweza kupatikana kwa kuwa na Dira ya Taifa itakayowaunganisha wote (Common Vision for All). Ni mapendekezo yangu kuwa dira hiyo ipatikane kwa kuandikwa Katiba mpya ya Zanzibar kupitia utaratibu utakaowashirikisha wananchi wote. Katiba hiyo mpya itafsiri upya misingi ya amana (trust) ambayo wananchi wanaipa mihimili mitatu ya Dola inayosimamia maongozi ya nchi – Mamlaka ya Utendaji (Serikali), Mamlaka ya Kutunga Sheria (Baraza la Wawakilishi) na Mamlaka ya Utoaji Haki (Mahkama). Wakishirikiana waongozi na waongowa, hakuna lisilowezekana. Cha kuzingatia ni wote kukubali kwamba “Politics is the art of the possible” (Siasa ni sanaa ya yanayomkinika) na “Politics is an art of compromise” (Siasa ni sanaa ya suluhu). Tukubali tu kuwa njia ya kusonga mbele ni kukubali kutofautiana katika fikra lakini tubaki kuwa wamoja. Uzalendo wa nchi utuunganishe. Tufahamu siasa si lengo, ni njia tu ya kufikia lengo. Lengo ni utumishi wa umma kwa kuyatimiza matarajio yao. Malengo ya utumishi huo wa umma ambayo ndiyo malengo ya Serikali yoyote inayothamini raia wake yanapaswa nayo kufafanuliwa na kuwa mwongozo wa Taifa. Yaliwekwa vizuri sana na Mzee Abeid Amani Karume katika Manifesto ya ASP ya 1961 katika kueleza tafsiri ya Uhuru unaopiganiwa: “UHURU ndio msingi wa siasa ya chama chetu. Unachanganya bila ya shaka kumalizika kwa Serikali ya Kikoloni na mwisho wa utawala wa nje. Kadhalika UHURU unakusanya ukunjufu kutokana na ujinga na haja zisizokwisha. UHURU wa kuwa na pato la kumwezesha mtu kuyatekeleza yaliyombidi, kustarehe na kuwa mtu, UHURU wa kuishi kama watu katika nchi yetu. Huu ndio UHURU ambao daima tukiutaka, huu ndio UHURU ambao daima twaupigania, huu ndio UHURU ambao tumejitolea kuutumikia na siku zote tutautumikia kwa nguvu zetu zote na kwa uwezo wetu wote. Tunadhani kuwa kila mmoja wetu katika visiwa hivi aendelee mbele kwa mujibu wa uwezo wake, jambo ambalo ni gumu lakini kabisa si jambo lisilowezekana. Na iwapo wewe kililahi huyapingi haya tuliyoadhimia na wewe mwenyewe ndiye uwezaye kujua, basi tafadhali karibu uungane nasi twende pamoja na kuutia mkononi huu UHURU.” Wazanzibari tunapaswa kujiuliza siasa tuliyo nayo kwa kiasi gani imetufikisha katika malengo hayo aliyoyaeleza Mzee Karume? Ni wangapi kati yetu tunaishi tukiwa na ukunjufu kutokana na ujinga na haja zisizokwisha? Ni wangapi tunamiliki pato la kumwezesha mtu kuyatekeleza yaliyombidi, kustarehe na kuwa mtu, kuishi kama watu katika nchi yetu? Ni wangapi kati yetu katika visiwa hivi tuna nafasi ya kuendelea mbele kwa mujibu wa uwezo wetu badala ya kutegemea ukoo gani tunaotoka? Je, tumefikia kiwango cha UHURU ambao daima tukiutaka, daima tukiupigania, na ambao tulijitolea kuutumikia na kuahidi kuwa siku zote tutautumikia kwa nguvu zetu zote na kwa uwezo wetu wote? Jawabu analo kila mmoja wetu. Uongozi ni utumishi wa umma. Umma lazima usimame kwa njia za amani kabisa kudai uadilifu wa uongozi kutoka kwa wanaowaongoza. Viongozi wakiona wananchi wamechachamaa watabadilika. Wasipobadilika watapeperushwa na upepo wa mabadiliko. Tukifikia hapo, heshima ya siasa kama fikra, busara na mipango ya kuendesha nchi itarudi.
HUO NDIO WARAKA,
Nina uhakika kwa kiasi fulani utakuwa umejifunza mengi yahusianayo na siasa pamoja na madaraka Tukirudi kwenye maneno ya prof. Shivji. Anaposema kuwa wanasiasa hawaipendi siasa lakini wanapenda madaraka, hapa mimi tafsiri yangu ni kwamba, siasa ni ngumu na pia inaweza ikamuweka mtu katika matatizo mbalimbali na kumnyima uhuru fulani na inaweza kumsababishia hatari katika maisha. Na maneno haya ni kweli kwa sababu ukiangalia na kuwatathmini maisha ya wapenda siasa na si wapenda madaraka wengi yalikuwa na misukosuko mingi na taabu. Mfano mkubwa wa mpenda siasa ni Raisi wa kwanza mzalendo wa Afrika ya kusini Nelson Mandela. Alitumia muda wake mwingi kufanya siasa za ukombozi kwa ajili ya taifa lake na hata mapambano hayo yakampelekea kufungwa jela kwa muda wa miaka 27, na hata alipo fanikiwa kupata uhuru hakukaa madarakani badala yake alikabidhi nchi kwa mtu mwingine. Kwa hiyo mtu ambaye anapenda siasa na si mwanasiasa ndio mpambanaji wa kweli kwani anapambana si kwa maslahi ya kupata madaraka, bali ni kwa ajili ya ukombozi wa kweli. Siasa huwapelekea wanasiasa wengi kupata madaraka mbalimbali katika nchi, hivyo watu wengi huingia kwenye siasa ili waweze kupata madaraka hayo. Pia mwanasiasa anapo pewa madaraka anakuwa na nguvu kubwa na mvuto kwa watu na pia husikilizwa na kuaminiwa. Hivyo unapokuwa unamadaraka fulani kupitia siasa,unatakiwa kutumia vizuri kwa manufaa ya jamii nzima. Lakini wapenda madaraka wengi hutumia fursa hii kujilimbikizia mali na kunyonya raslimali za nchi.
REJEA:
- - Marcus Tullius Cicero, The Republic, kama ilivyonukuliwa katika Chris Paten (1998), East and West, Macmillan (London).
- - John Uhr (2003), ‘Creating a Culture of Integrity’, The Second Publication in the series “Taking Democracy Seriously”, Commonwealth Secretariat (London).
- - Kieron O’Hara (2004), Trust: From Socrates to Spin (Icon Books: Cambridge).
- - Jean-Jacques Rousseau (1993), The Social Contract and Discourses (trans. G.D.H. Cole, rev. J.H. Brumfitt and John C. Hall, upd. P.D. Jimack) (Everyman: London)
- - Brian Skyrms (1996) Evolution of the Social Contract (Cambridge University Press: Cambridge).
- - Rudolph Giuliani (2002), Leadership (Little, Brown, London).
- - Abdilahi Nassir (1991), ‘Liberation Theology: The Islamic Perspectives’ , Waraka uliowasilishwa katika Mkutano wa Kimataifa wa kujadili Ukombozi wa Pili wa Bara la Afrika, uliofanyika Februari 1991 mjini London.
- - How will history judge him?’, The Economist (London), May 12th – 18th 2007. - Salmin Amour (1999), Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Salmin Amour kwenye Karamu Rasmi ya kutiwa saini Makubaliano baina ya CCM na CUF, Ikulu
- – Zanzibar tarehe 9.6.99, (Government Printers, Zanzibar). - Fareed Zakaria (2003), The Future of Freedom: Illiberal Democracy at Home and Abroad (W.W. Norton & Company, New York, London). - Abeid Amani Karume (1961), Manifesto ya ASP, (Zanzibar).
No comments:
Post a Comment